Matthew 27:1-14

Yesu Aletwa Mbele Ya Pilato

(Marko 15:1; Luka 23:1-2; Yohana 18:28-32)

1 aAsubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. 2 bWakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.

Yuda Ajinyonga

(Matendo 1:18-19)

3 cYuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4 dAkasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”

5 eBasi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

6 fWale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” 7Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. 8 gHii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. 9 hNdipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, 10 iwakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

Yesu Mbele Ya Pilato

(Marko 15:2-15; Luka 23:3-25; Yohana 18:33–19:16)

11 jWakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”

12 kLakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. 13 lNdipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” 14 mLakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

Copyright information for SwhNEN